Makubaliano ya kusitisha vita nchini Ukraine yameheshimiwa kwa kiasi kikubwa, licha ya kwamba mapigano yamezuka tena katika mji wa Debaltseve. Kwa mujibu wa shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya, milio ya mizinga ilisikika kwa muda upatao saa moja. Mapigano yameripotiwa pia katika miji ya Luhansk na Raihorodka, yote Mashariki mwa Ukraine. Marekani inaishutumu Urusi kwa kupeleka silaha katika eneo hilo, suala ambalo Urusi imekanusha. Nayo serikali ya Ujerumani katika tamko lake imeelezea wasiwasi juu ya hali tete ya usalama mjini Debaltseve. Makubaliano ya kuweka silaha chini yalifikiwa baada ya mkutano kati ya viongozi wa Ujerumani, Ufaransa, Urusi na Ukraine mjini Minsk, Belarus. Viongozi hao leo watajadiliana kuhusu hatua zaidi za kuchukua ili kuleta amani ya kudumu.
Na huko Yemen Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limewataka mashia wa jamii ya Houthi ambao wanatetea demokrasia nchini Yemen waachie madaraka na pia kumwachia huru rais Abedrabbo Mansour Hadi. Wanachama wote wa baraza la usalama walipitisha azimio ambalo lilipendekezwa na Uingereza na Jordan. Hata hivyo, kabla ya baraza la usalama kupigia kura azimio hilo, mashia wa Huthi waliweka wazi kwamba hawako tayari kung'atuka, licha ya kuwekewa shinikizo na Umoja wa Mataifa na nchi za Kiarabu. Jumuiya ya nchi za Kiarabu imeitisha mkutano wa maafisa wake wa kidiplomasia ambao utafanyika Jumatano hii. Mashia wa Houthi walitwaa madaraka nchini Yemen mapema mwezi huu baada ya kuiteka ikulu na jambo lililopelekea rais pamoja na serikali yake kujiuzulu. Serikali ya Yemen ilikuwa na mpango wa kuigawa ardhi ya Yemen kwa misingi ya kimadhehebu, sehemu iwe ya Masuni na sehemu nyingine ya MaShia, jambo ambalo lingeleta hatari kubwa sana katika taifa hilo.